Events & News
Mnzava atembelea mradi wa jengo la mama na mwana Haydom
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto Hospitali ya Rufaa Haydom. “Tumekagua jengo na nyaraka na tumeridhika. Tuko tayari kuweka alama ya kwamba tulipita katika eneo hili na kuweka kibao cha kutembelea. Tunawatakia kila lakheri katika kutekeleza majukumu yenu na matumaini yetu, na ndio Imani ya serikali, kwamba ujenzi huu utakamilika kama mlivyo eleza na mwezi Machi, 2025 lianze kutoa huduma kwa mama na mtoto,” alisema Mnzava. Tukio hilo limeshuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Fatma Hamad Rajab, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Dkt. Mwiga Mbesi, Mkurugenzi Maendeleo ya vijana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shaibu Ibrahim. Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Bi. Veronica Kessy, Mkurugenzi wa utawala na Rasilimali Watu Hospitali ya Kilutheri Haydom Ndugu Bariki Kibona alisema ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 51.8; na unategemea kukamilika mwezi Machi mwakani. “Mpaka sasa ujenzi wa jingo la mama na mtoto limekamilika kwa asilimia 51.8 ambapo sehemu ya chini (basement), sehemu ya ardhi (ground floor) na ghorofa ya kwanza zimejengwa na ziko hatua ya ukamilishaji. Aidha lengo la mradi ni kujenga ghorofa 2,” alifafanua ndugu Kibona. Alieleza yakua gharama za ujenzi wa jengo hilo ni shilingi 4,600,000,000 ambapo chanzo cha fedha zote ni mapato ya ndani ya hospitali. Hadi sasa mradi umetumia kiasi cha shilingi 1,700,000,000. Ndugu Kibona alisema faida za mradi utakapokamilika yakua ni pamoja na kuwezesha huduma ya mama na mtoto kutolewa katika mazingira mazuri yenye usiri unaotakiwa. “Mradi huu pia utasaidia kutoa huduma kwa idadi kubwa ya akina mama na watoto; na kwasasa umewezesha upatikanaji wa ajira kwa wananchi na kuongeza kipato kwa mamantilie na wafanyabiashara,” alisema ndugu Kibona. Ndugu Kibona alifafanua yakua hospitali iliamua kutekeleza mradi huo kutokana na ongezeko la wagonjwa na uchakavu wa miundombinu iliopo, kwani hospitali inahudumia wagonjwa wa nje Zaidi ya 100,000 na wagonjwa wa ndani Zaidi ya 11,000 kwa mwaka. Hospitali pia inahudumia wajawazito Zaidi ya 25,000 na vizazi zaidi ya 3,800 kwa mwaka. .